December 2010
Kaimu mkuu wa mkoa wa Iringa Bi.Evarista kalalu akitosa salamu za ufunguzi wa Mkesha ulioandaliwa na umoja wa makanisa Tanzania

Askofu wa KKKT Dayosisi ya Iringa Dk Mdegella akiendesha maombi maalum ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2011
Wananchi wakiwa katika mkesha
uwanja wa samora usiku huu

Shughuli za mkesha wa mwaka mpya Iringa
Dua ya kuomba heri ya mwaka mpya.
Picha zote na mdau mkuu wa Iringa Francis Godwin

no image
Ankal!
Naomba uniazime sh 300,000 tu nina shida nazo hasa kesho...Nitarudisha baada ya Ijumaa ya next wk! Help me plz, i know u hav them. Alisikika mlevi mmoja akiiomba mashine ya ATM saa 6 usiku leo!! Khaa! Ulivyostuka ulifikiri nakuomba wewe, ukaanza kuandaa fiksi za kunitolea nje.
I wish u happy New Year 2011!
From Mdau
Sent from my BlackBerry® wireless device
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein, akitoa salamu za mwaka mpya wa 2011 kwa wananchi wa Zanzibar,
kwa kuwatakia kheri ya mwaka mpya, kuwa na Amani na Utulivu,bila ya kuwa na migogoro ya aina yoyote. Picha na mdau Ramadhan Othman wa Ikulu Zanzibar.

Waheshimiwa wadau,

Kwa heshima na taadhima natoa salamu za MWAKA MPYA wa 2011 kwa wadau wote popote mlipo ulimwenguni. Nitakuwa mtovu wa fadhila endapo kama sintosema kwamba bila ninyi Libeneke lisingenoga. Asanteni sana na nawashukuru kwa kampani mnayonipa na mliyonipa toka Septemba 5, 2005 nilipozindua rasmi Globu ya Jamii kule Helsinki, Finland, chini ya usimizi wa mdau mkuu kaka Ndesanjo Macha.

Leo tunauanza mwaka mpya tukiwa na kila aina ya matumani kwamba Mola atatujaalia si pumzi tu bali pia fanaka katika kila jambo la maendeleo wakati tukianza ngwe hii mpya ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Nina mengi ya kusema, ila endapo nitathubutu kufanya hivyo nahisi nitajaza ukurasa wote huu lakini bado nisiweze kueleza robo tu ya niliyonayo moyoni. Itoshe tu niseme asanteni wadau wote kwa kuendelea kuniunga mkono kwenye shida na raha, katika kukubaliana na katika kupingana bila kupigana. Asanteni sana, sana, sana wadau wa Globu hii ya Jamii.

Sina zaidi ya kuahidi kwa mwaka mpya zaidi ya kuendeleza Libeneke kama kawaida. Hivi sasa nimejipanga kuja na mpya kadhaa ikiwa ni pamoja na mahojiano na watu wanaotakiwa kutoa neno katika lolote linalosibu jamii katika wakati husika, ikiwa ni kwa maandishi na video. Nitakaribisha pia fursa ya wadau kudai nani wa kumhoji na juu ya nini katika mfumo huo mpya ambao Globu ya Jamii itakuja nao kwa jina la MASWALI KUMI KWA......

Napenda pia kukumbusha sera ya Globu ya Jamii ya kwamba ‘Kilicho chema kwa bata mzinga, si chema kwa kuku’ (what’s good for the goose, is bad for the hen) yaani si rahisi kumridhisha kila mmoja kati ya wadau milioni moja na nusu wanaotembelea Globu ya Jamii kwa siku. Hivyo nawataka radhi kabisa wale ambao nitakuwa siwaridhishi kwa namna moja ama nyingine, na kwamba hiyo si kwa makusidi bali ni hali halisi ya maisha. HAKUNA ALIYE MKAMILIFU ILA MOLA PEKEE. Kwa hiyo maoni yako yakitiwa kapuni ujue ni katika hilo. Nia ni ile ile ya kupashana bila kuwa na haja ya kujeruhi mtu ama watu kwa kuchafua hali ya hewa.

Wakati ni kweli kwamba mwaka 2011 una changamoto (challenges) kibao katika tasnia hii ya libeneke, lakini si uwongo kwamba kwa msaada wenu wadau hali inaweza kuboreshwa zaidi. Na hii itawezekana endapo kama sie sote tutatumia teknolijia hii ya habari kwa kuendeleza maendeleo ya nchi na si mtu binfasi ama kikundi Fulani cha dini, siasa ama jamii.

Katika hilo nafurahi na kuona fahari kubwa kwamba Globu ya Jamii imekuwa chachu ya kuanzishwa Libeneke nyingi nchini na nje ya nchi zenye kuwa na msimamo wa kupashana habari kwa njia ya kisasa. Ushahidi ni jinsi ambavyo Globu ya Jamii ilivyo mstari wa mbele katika kutangaza blog mpya zinazoanzishwa kila ikitokea hivyo.

Pamoja na yote hayo nina masikitiko makubwa kwamba blogu nyingi zinazoanzishwa zinakuwa ni zile zile tu, kama zetu za akina sie. Yaani kwa mtazamo wa wengi blogu ni kuwa na habari za kila mara ama kila siku, badala ya wanaoanzisha blogu kujikita katika fani ambazo wamebobea. Badala ya wote kujikita katka katika habari, tunahitaji blogu za Nyanja tofauti zaidi ya habari tu. Kwa mfano tunahitaji blogu za useremala, uashi, urembo ama hata muziki wa mipasho. Si kila aanzishaye blogu ajikite katika habari na kutaka kutunishana misuli na kina sie tulio ndani ya tasnia ya habari. Angalizo hapa ni kwamba copy & paste aghalabu hukimbiza wasomaji.

Mwisho napenda kutoa shukurani kwa wote walioifanya Globu ya Jamii ifike hapa ilipo leo. Ni ngumu kumtaja kila mmoja. Lakini si vibaya nikiwataja baadhi ambao wamenipa msukumo kuendeleza Libeneke.

Naomba nianze na mdau mkuu Ndesanjo Macha aliyenifungua macho na kuanza kublogu, wa pili ni kaka yangu mpendwa aliye huko Helsinki, Finland, Fidelis Tungaraza aka Mti Mkubwa (Fide nashukuru sana kwa ushauri wako wa kila mara) , Jeff Msangi wa Canada, Balozi Peter Kallaghe na Balozi Mwanaidi Maajar (Mama maajar alinialika London kutoa mada ya Libeneke katika Disapora II, asante sana mama Maajar kwa kutambua mchango wetu katika jamii, mwaliko wako London umenipa moyo sana kuendeleza Libeneke), Balozi Patrick Tsere, Maggid Mjengwa, Haki Ngowi, Francis Godwin (asante na hongera kwa kuendeleza Libeneke huko Iringa) wadogo zangu Ahmad na Othman Michuzi, Mh. Lazaro Nyalandu, Dk. Emmanuel Nchimbi, Mh. Amos Makalla, kak Gardol wa Reading, Da'Chemi Che-Mponda, Shamim Mwasha 'Zeze', Zubeir Masabo, Lau Shari wa Arise na juu ya yote mke wangu Ainde na Rais Jakaya Mrisho Kikwete (nashukuru sana mheshimiwa Rais kwa kunipa moyo wa kutembelea kwako blogu zetu mbalimbali kila siku, unatutia moyo sana kwa kweli).

Naomba pia niwashukuru wadhamini wakuu wa Globu ya Jamii wakiongozwa na Vodacom Tanzania, Tanzania Breweries Limited, CRDB, LUCUS, Hillview Family, TIB, Export Showroom, IOM ambao bila wao tusingekuwa hapa leo.

Mwisho na mwanzo ni MK Computer Tweaks ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kwamba tuna blogu zenye muonekano wa kimataifa, chini ya kaka Christopher Makwaia. Asante sana MK kwa yote uliyoifanyia Globu ya Jamii na unayoendelea kuifanyia. Mola akuzidishie!

HERI YA MWAKA MPYA MDAU POPOTE ULIPO

Muhidin Issa Michuzi

no image
SALAM ZA MWAKA MPYA ZA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHESHIMIWA DKT.JAKAYA MRISHO KIKWETE KWA WATANZANIA,
TAREHE 31 DESEMBA, 2010

Ndugu Wananchi;
Habari za jioni.
Leo tunauaga Mwaka 2010 na kuukaribisha Mwaka 2011. Kama ilivyo ada, hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, kwa kutujaalia uhai na kutuwezesha kuifikia siku hii adhimu. Wapo ndugu, jamaa na marafiki zetu wengi ambao hawakujaaliwa bahati hii kwa kuwa wametutangulia mbele ya haki. Tuzidi kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awape mapumziko mema.

Ndugu Wananchi;

Kwa namna ya kipekee mimi binafsi, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia uzima na kuniwezesha kuendelea kuitumikia nchi yangu na ninyi wananchi wenzangu. Nawashukuruni sana wananchi wenzangu kwa kuendelea kuniunga mkono mimi na kuiunga mkono Serikali yetu ninayoiongoza. Mmefanya hivyo mwaka huu tunaoumaliza leo na tangu tuingie madarakani miaka mitano iliyopita mpaka sasa. Imani na upendo mliyotuonesha vimetupa faraja na ari ya kuendelea kuwatumikia kwa bidii zaidi. Nawaomba muendelee na moyo huo katika mwaka mpya tunaoukaribisha usiku wa leo. Mimi nawaahidi kuendelea kutumia vipaji vyangu vyote nilivyojaaliwa na Mwenyezi Mungu kuwatumikia wakati wote na kwa hali yoyote kama nilivyofanya mwaka huu tunaoumaliza leo na miaka ya nyuma.

Ndugu wananchi;

Mwaka 2010 ulikuwa na shughuli nyingi na mafanikio mengi licha ya kuwepo changamoto mbalimbali zilizojitokeza. Kwa ajili hiyo tunaingia mwaka 2011 tukiwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri zaidi.
Hali ya Usalama Nchini

Ndugu Wananchi;

Hali ya usalama wa nchi yetu ni mzuri, mipaka iko salama na hakuna tishio lolote kutoka mahali popote au watu wowote linalotia mashaka. Uhalifu umeendelea kudhibitiwa na mafanikio yamekuwa yanapatikana. Taarifa ya Jeshi la Polisi ya hivi karibuni inaonyesha kuwa matukio ya uhalifu yamepungua mwaka huu ukilinganisha na mwaka uliopita.

Ndugu Wananchi;

Ni jambo la kujivunia kwamba tumemaliza mchakato wa uchaguzi mkuu kwa amani na salama. Tulikuwa na siku 70 za kampeni, moja ya kupiga kura na siku 6 za kusubiri matokeo bila ya kuwepo matukio ya uvunjifu wa amani yanayostahili kuzungumzwa. Sehemu zetu zote mbili za Muungano kulikuwa salama na Zanzibar ndiko kulikuwa na utulivu mkubwa zaidi kuliko miaka ya nyuma.

Hakika Tanzania tumeendelea kudumisha sifa yetu ya kuwa kisiwa cha amani na utulivu. Naomba sote tujipongeze, lakini tutoe pongezi maalum kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya mwaka huu ya kuhakikisha kuwa nchi yetu na watu wake wako salama.
Demokrasia Inazidi Kuimarika

Ndugu Wananchi, Watanzania Wenzangu;

Mwaka huu tumeshuhudia demokrasia ilivyozidi kuota mizizi, kukomaa, kustawi na kuimarika. Tumefanya Uchaguzi Mkuu wa nne chini ya mfumo wa vyama vingi kwa mafanikio makubwa. Sisi wenyewe ni mashahidi na dunia nzima ni mashahidi wa ukweli huo. Wakati tukitambua na kujipongeza kwa mafanikio haya, hatuna budi kujiwekea dhima ya kufanya mambo yetu vizuri zaidi katika chaguzi zijazo. Tufanye tathmini ya uchaguzi wetu uliopita ili tuimarishe na kudumisha yaliyo mazuri na kurekebisha yenye mapungufu.

Ndugu Wananchi;

Uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa na ushindani mkali na nguvu ya vyama vya upinzani imeongezeka. Hili ni jambo jema kwa utawala bora na uwajibikaji nchini. Bila ya shaka Bunge litachangamka kama tunavyotarajia sote. Nimewakumbusha Mawaziri wajibu wao wa kuwa makini na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi Bungeni. Kwa upande wa Chama tawala hatuna budi kujipanga na kujijenga upya kwa kuzingatia mazingira mapya ya kisiasa nchini.

Ndugu Zangu, Watanzania Wenzangu;

Naomba kurudia kukumbusha kuwa uchaguzi ulishaisha Oktoba 31, 2010 na malumbano ya kampeni za uchaguzi yalimalizika wakati ule. Sasa ni wakati wa kuendelea kufanya shughuli zetu za kawaida za kujiletea maendeleo yetu wenyewe na ya nchi yetu. Kuendeleza malumbano na kuendelea kuishi kama vile kampeni za uchaguzi bado zinaendelea siyo sahihi hata kidogo.
Najua wapo baadhi ya wanasiasa na vyama vya siasa ambavyo vimepanga mikakati ya kuendeleza malumbano ya uchaguzi na kutaka Watanzania waishi kama vile nchi ipo kwenye kampeni za uchaguzi. Wamepanga wakati wote kutafuta jambo au hata kuzua jambo ili kuwachochea wananchi waichukie Serikali. Wamepanga kuchochea migomo vyuoni na maandamano ya wananchi mara kwa mara. Kwao wao huo ndiyo mkakati wa kujijenga kisiasa ili kujiandalia ushindi kwenye uchaguzi wa mwaka 2015.

Nawatanabaisha ndugu zangu myajue hayo ili msipoteze muda wenu muhimu wa kujiendeleza na kugeuzwa kuwa mbuzi wa kafara kwa ajili ya kuendeleza maslahi ya kisiasa ya watu fulani. Kwa jinsi watu hao walivyokuwa wabinafsi na wasivyokuwa na huruma na wenzao, wako tayari kuchochea ghasia bila kujali madhara yatakayowakuta watu watakaoshiriki. Wao hasa wanachotaka ni ghasia kutokea na vyombo vya dola kuingilia ati waiambie jumuiya ya kimataifa jinsi Serikali yetu ilivyo katili. Nawasihi ndugu zangu msiwasikilize wala kuwafuata wanasiasa hawa.
Nawaomba, wakiwafuata wakumbusheni kuwa wao wanazo fursa nyingi za kusema wayatakayo Bungeni na kwingineko, waache kuwatumia kama chambo au wahanga wa maslahi yao.

Uwajibikaji wa Mawaziri

Ndugu wananchi;
Tunaumaliza mwaka 2010 na kuukaribisha mwaka 2011 tukiwa na Serikali mpya yenye damu mpya nyingi na changa katika Baraza la Mawaziri. Nimejitahidi kuwapanga Mawaziri hao kwa namna ambayo wanaweza kutumia vyema maarifa yao na uzoefu wao kulisukuma kwa kasi, ari na nguvu zaidi, gurudumu la maendeleo ya nchi yetu. Nimeshakutana na kuzungumza nao wote kuhusu majukumu yao na wajibu wao.

Nimewasisitizia matumaini yangu kwao ya kuwa wachapa kazi hodari na kupiga vita rushwa, uzembe na ubabaishaji bila ya ajizi. Wawe watu waaminifu na waadilifu, watakaochukia maovu na kuyapiga vita kwa nguvu zao zote katika maeneo yao ya kazi. Wawe ni watu wenye moyo wa kuipenda nchi yetu na watu waliotayari kuitumikia kwa moyo na uwezo wao wote. Wawe karibu na watu wawasikilize na wawe wepesi kutatua shida zao. Aidha, nimewakumbusha kutambua kuwa ahadi kubwa ya CCM kwa Watanzania ni Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010, hivyo wahakikishe kuwa malengo ya Ilani kuhusu maeneo yao ya uongozi wanayatambua vizuri na kuyapangia mipango thabiti ya utekelezaji na kufuatilia kwa dhati utekelezaje wake. Nafurahi kwamba Mawaziri tayari wameanza kazi kwa kasi nzuri na wengine kwa kishindo. Naomba tuendelee kuwaunga mkono na kuwasaidia.

Nidhamu ya Matumizi

Ndugu Wananchi;
Miongoni mwa mambo ambayo nimesisitiza kwa Mawaziri ni kuhakikisha kuwa wanasimamia vizuri ukusanyaji wa mapato ya Serikali na hasa nidhamu ya matumizi ya fedha na mali za umma. Tunapata mafanikio ya kutia moyo kwa upande wa ukusanya mapato. Ndugu zetu wa TRA wanastahili pongezi zetu kwa kazi waifanyayo. Pamoja na hayo hatuna budi kuongeza mapato ya Serikali maradufu juhudi zetu za kukusanya mapato, kwani mahitaji yanazidi kuongezeka wakati uwezo wa mapato hauongezeki kwa kasi hiyo hiyo.

Ndugu Wananchi;

Kwa upande wa nidhamu ya matumizi bado hatujapiga hatua ya kunifanya nipoe moyo, ingawaje kuna mafanikio yanayoendelea kupatikana. Niliwakumbusha Mawaziri kuhusu kuwepo Kamati za Matumizi ya Fedha katika kila Wizara, Idara za Serikali na Halmashauri za Wilaya na Miji ambazo niliagiza ziundwe miaka mitatu iliyopita. Niliwakumbusha kuwa, wakuu wa taasisi hizo ndio wanaoongoza Kamati hizo na hivyo wao ndiyo wanaoongoza Kamati za Wizara zao. Nimewataka wahakikishe kuwa Kamati hizo zinatekeleza ipasavyo majukumu yake ili rasilimali za taifa zifanye kazi iliyokusudiwa. Halikadhalika, niliwataka wahakikishe kuwa Kamati za Idara na Mashirika chini ya Wizara zao zinafanya kazi kwa ukamilifu.

Ndugu Wananchi;

Kwa upande wa Halmashauri za Wilaya na Miji, mwaka huu tuliendelea kuziimarisha Idara za Uhasibu na Ukaguzi wa Ndani. Tutaendelea kuhakikisha kuwa kila Halmashauri ina Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani wenye ujuzi na sifa zinazostahili za kitaaluma, uaminifu na uadilifu.

Siku za nyuma tulishafanya uamuzi wa kumfanya Mhasibu Mkuu wa Serikali kuwa na mamlaka ya kuangalia utendaji wa shughuli za fedha katika Halmashauri za Wilaya na Miji kama aliyonayo kwa Wizara na Idara za Serikali Kuu. Mwaka huu tumeamua kuwaunganisha Wakaguzi wote wa Ndani wa Wizara na Idara za Serikali chini ya Uongozi mmoja. Aidha, tumeunda nafasi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani ambaye Wakaguzi wa Ndani wote wa Wizara na Idara za Serikali watakuwa chini yake na kuwajibika kwake. Yeye atahusika na uteuzi wao na kuwapangia vituo. Tumeamua, pia, kuwa Mkaguzi Mkuu wa Ndani atakuwa na mamlaka kwa Wakaguzi wa Ndani wa Halmashauri za Wilaya na Miji. Bila ya shaka hatua hii itasaidia kuimarisha uwajibikaji, nidhamu na uaminifu katika matumizi ya pesa na mali za umma.

Hali ya Uchumi

Ndugu Wananchi;
Tunaumaliza mwaka 2010 hali ya uchumi wa nchi ikiwa ni ya kuridhisha. Inaelekea athari za miaka mitatu iliyopita zilizosababishwa na misukosuko mbalimbali ya uchumi wa dunia sasa zinanza kutoweka. Tunatarajia kuwa mwaka huu uchumi utakua kwa asilimia 7 ukilinganisha na asilimia 6 ya mwaka 2009. Matumaini yetu ni kuwa mwaka 2011 uchumi utakua kwa asilimia 7.2 kama mambo yatakwenda kama tunavyotarajia.

Mfumuko wa bei nao umeshuka sana kutoka wastani wa asilimia 12.1 mwaka 2009 hadi asilimia 5.5 Novemba, 2010. Ni dhamira yetu na matarajio yetu kuwa mfumuko wa bei utaendelea kuwa chini ya hapo. Kwa ajili hiyo hatuna budi kuhakikisha kuwa hali ya ipatikanaji wa chakula nchini inaendelea kuwa nzuri.

Kilimo na Chakula

Ndugu wananchi;
Hali ya upatikanaji wa chakula nchini ilikuwa nzuri katika mwaka 2010 lakini hatuna hakika hali itakuwaje katika mwaka 2011. Tunazo sababu za kutia shaka kwa sababu ya hali ya mvua kutokuwa nzuri katika maeneo mengi hapa nchini. Maeneo mengi yanayopata mvua za vuli katika mikoa ya Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara hali ilikuwa mbaya. Mvua zimekuwa pungufu sana na wakulima wengi hawakudiriki hata kupanda mazao. Kwa mikoa hii matumaini yetu tunayaweka kwa mvua za masika zinazotarajiwa kuanza kunyesha mwezi Machi. Tuombe kwa Mola mvua zipatikane za kutosha tunusurike na baa la njaa.

Ndugu Wananchi;

Kwa upande wa Mikoa ya Kusini Nyanda za Juu na mingineyo inayopata mvua moja kuanzia mwezi Novemba au Desemba, mvua zilichelewa kuanza kunyesha. Hivi sasa zimeanza na zinaendelea vizuri. Tuzidi kumuomba Mungu ziendelee vizuri ili taifa liwe na hakika ya akiba ya kutosha ya chakula ambayo huchangiwa kwa zaidi ya asilimia 85 na mikoa ya ukanda huu.
Wataalamu wetu wa Idara ya Hali ya Hewa wametahadharisha kuwa hata maeneo haya huenda yakapata mvua chini ya kiwango cha kawaida. Kwa ajili hiyo, niwaombe ndugu zangu wa mikoa ya Iringa, Ruvuma, Mbeya na Rukwa kuhakikisha kuwa wanazitumia vizuri mvua zinazonyesha sasa. Tukifanya hivyo athari za upungufu wa mvua tutazipunguza. Na, kwa wananchi wote kwa jumla nawaomba tuwe waangalifu katika matumizi ya akiba yetu ya chakula tuliyonayo. Wahenga walisema “tahadhari kabla ya hatari”. Tuzingatie maneno hayo ya hekima.

Hifadhi ya Chakula

Ndugu Wananchi;
Mwaka 2010 tumeamua kuongeza akiba yetu ya chakula katika Hifadhi ya Taifa ili ifikie tani 400,000 ifikapo mwaka 2015. Tumeanza safari hiyo kwa dhati. Mwaka huu tumenunua tani 200,000 na kuzihifadhi. Kwa sababu hiyo tuliongeza fedha za kununulia chakula kutoka shilingi bilioni 18.2 hadi shilingi bilioni 60.26. Tutaendelea kukuza uwezo huo mpaka tufikie lengo letu.

Pembejeo za Kilimo

Ndugu Wananchi;
Mwaka huu tumeongeza mbolea ya ruzuku na wakulima wengi zaidi watapata mbolea hiyo. Tutaendelea kufanya hivyo katika miaka ijayo kwa lengo la kuwafikia wakulima milioni 3.5 mpaka 4 miaka mitano ijayo. Aidha, tutaendelea kufuatilia na kuyatafutia ufumbuzi matatizo ya upatikanaji na hasa usambazaji wa pembejeo kwa wakulima na wafugaji. Nasikitishwa sana na taarifa za vitendo vya wizi na udanganyifu vinavyofanywa na baadhi ya mawakala wa mbolea, mbegu na dawa za kilimo na mifugo wakishirikiana na baadhi ya watumishi wa umma wa ngazi mbalimbali.

Nimewataka Mawaziri husika na hasa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya na vyombo vya dola yaani Polisi na TAKUKURU kufuatilia mwenendo mzima wa usambazaji na upatikanaji wa mbolea, mbegu na dawa za ruzuku kwa wakulima na wafugaji. Wawatafute na kuwabaini wale wote wanaofanya vitendo viovu kinyume na taratibu zilizowekwa na kuwachukulia hatua za kisheria na kinidhamu. Watu hawa ni wahujumu wa uchumi, ni adui wa wakulima, wafugaji na taifa zima kwa jumla. Hawastahili na wala wasionewe huruma hata chembe.

Ndugu wananchi;

Pamoja na mikakati tuliyojiwekea ya kuboresha kilimo, tutaendelea kuwekeza na kuhamasisha uwekezaji katika sekta nyingine ambazo tunazitegemea zisaidie kukuza uchumi na kupunguza umaskini kama vile viwanda, utalii, biashara, miundombinu ya barabara, reli, bandari, umeme, maji n.k. Kwa upande wa huduma ya fedha, Serikali itaendelea kuongeza mtaji kwenye Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) ili irudie kuwa benki ya maendeleo na kutoa mikopo ya muda wa kati na mrefu kwa wawekezaji wetu. Ni dhamira yetu kuwa mwaka 2011 tuongeze kasi ya kuanzisha Benki ya Kilimo ili ikiwezekana ianze au matayarisho yafikie hatua nzuri ya kuweza kuanza mwaka unaofuata.

Matatizo ya Umeme

Ndugu wananchi;
Mwaka 2010 haukuwa na utulivu wa kutosha kwa upatikanaji wa umeme. Mara kadhaa kumekuwepo na matukio ya kukatika na mgao wa umeme kutokana na uharibifu wa mitambo ya kuzalisha umeme hasa katika kituo cha Songas na vituo vya TANESCO. Pamoja na hayo tatizo la msingi ni uwezo wa uzalishaji wa umeme kuwa mdogo kuliko mahitaji. Hivyo basi, hitilafu katika mtambo mmoja au kituo kimoja cha kuzalisha umeme huzua tatizo kubwa la upatikanaji wa umeme kwa nchi nzima.

Ndugu Wananchi;

Katika kukabiliana na tatizo hilo miaka mitano iliyopita, TANESCO kwa msaada wa Serikali, imeongeza uwezo wa kuzalisha umeme kwa MW 145 (MW 100 Ubungo na MW 45 Tegeta) kwa kutumia gesi asilia. Bahati mbaya mpango wa kuzalisha MW 300 kule Mtwara kwa kushirikiana na sekta binafsi, haukufanikiwa baada ya mwekezaji kushindwa kupata fedha kwa sababu ya mgogoro wa masoko ya fedha ya kimataifa. Kama tatizo hilo lisingekuwepo umeme huo ungekuwa unakamilika au kukaribia kutumika hivi sasa.

Kwa sasa TANESCO ina mipango kadhaa inayoendelea nayo ya kuongeza uzalishaji wa umeme nchini. Kwa msaada wa Serikali ndani ya miezi 12 ijayo, TANESCO itaongeza uzalishaji wa umeme kwa MW 160, (MW 100 Ubungo kwa kutumia gesi asilia na MW 60 Mwanza kwa kutumia dizeli nzito). Kwa kushirikiana na sekta binafsi pia, ndani ya miezi 36 ijayo TANESCO wanatarajia kukamilisha ujenzi wa vituo vya umeme huko Kinyerezi (MW 240) Somanga Fungu (MW 230) na Mtwara (MW 300). Inatarajiwa pia kwamba katika kipindi hicho mradi wa kuzalisha MW 200 pale Kiwira utakamilika.

Bei ya Umeme

Ndugu Wananchi;
Natambua kuwepo kwa mazungumzo, katika jamii kuhusu uamuzi wa EWURA wa kukubali ombi la Shirika la Umeme (TANESCO) kuongeza bei ya umeme. Wakati mwingine mazungumzo yamekuwa na hisia kali na hata jazba kutawala. Wizara, TANESCO na EWURA wameeleza kwa ufasaha misingi iliyotumika mpaka kufikia uamuzi huo. Sina maelezo mazuri zaidi ya hayo. Ninachotaka kusema mimi ni kuwaomba Watanzania wenzangu kutokukubali suala hili la kibiashara na kiuchumi kugeuzwa kuwa la kisiasa na kutafutiwa majawabu ya kisiasa.

Naomba tuamini na kukubali maelezo ya TANESCO na EWURA kwamba katika miaka minne hii gharama za uendeshaji, uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme zimepanda kama zilivyopanda katika shughuli nyingine. Hivyo basi, kutaka bei ya umeme ibaki kama ilivyokuwa miaka minne iliyopita hautokuwa uamuzi sahihi kiuchumi na kibiashara kwa TANESCO. EWURA imefanya kazi nzuri ya kuchambua maombi ya TANESCO na kuyakubali yanayostahili na kuyakataa yasiyostahili kuwa sehemu ya bei. Kwa kufanya hivyo, watumiaji wa umeme wamelindwa wasibebeshwe mzigo usiostahili na Shirila la Umeme limewezeshwa ili lisiendeshe shughuli zake kwa hasara.

Mahusiano ya Kimataifa

Ndugu Wananchi;
Katika mwaka 2010 Serikali iliendelea na jitihada za kupigania na kuendeleza maslahi ya Tanzania miongoni mwa mataifa duniani na mashirika ya kimataifa na kikanda. Kazi hiyo tumeifanya kwa mafanikio na faida zake tunaziona. Tumeshuhudia kuongezeka kwa misaada ya maendeleo, kupatiwa misamaha ya madeni, kuongezeka kwa wawekezaji na mitaji kutoka nje na kuzidi kuongezeka kwa watalii. Aidha, mauzo yetu nje pamoja na mapato na akiba yetu ya fedha za kigeni navyo vimeendelea kuongezeka.

Jina la nchi yetu limeendelea kung’ara katika medani za kimataifa. Tanzania imeendelea kushirikishwa katika masuala muhimu ya kikanda na kimataifa. Kwa mfano, Rais Mstaafu, Mheshimiwa Benjamin W. Mkapa aliteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuongoza Tume ya kuangalia mchakato wa kura ya maoni ya Sudan ya Kusini itakayofanyika tarehe 9 Januari, 2011.

Katika kura hiyo, wananchi wa Sudan ya Kusini wataamua iwapo wawe taifa huru au waendelee kuwa sehemu ya Sudan kama ilivyo sasa na Wananchi wa Jimbo la Abyei watapiga kura ya kuamua wawe upande upi: Sudan Kusini au Sudan Kaskazini. Tunamtakia heri Rais Mstaafu Benjamin Mkapa ili akamilishe jukumu hilo kwa mafanikio. Wakati huo huo tunawatakia wananchi wa Sudan ya Kusini na Sudan, kwa jumla, kuendesha zoezi hilo kwa amani na salama ili watu wapate fursa ya kuamua matakwa yao kwa uhuru.

Ndugu Wananchi;

Katika mwaka huu tunaoumaliza leo Umoja wa Mataifa umetupatia heshima nyingine kubwa. Shirika la Afya Duniani limeniteua mimi na Waziri Mkuu wa Canada Mheshimiwa Stephen Harper kuwa Wenyeviti Wenza wa kuongoza Tume ya Kimataifa kuhusu Afya ya Akina Mama na Watoto. Lengo kuu la Tume hiyo ni kuzisaidia nchi zinazoendelea ziweze kutekeleza Malengo ya Milenia kuhusu kupunguza vifo vya akina mama na watoto.

Tume yetu ina kazi ya kupendekeza mfumo wa kutoa taarifa juu ya maendeleo ya afya za akina mama na watoto na kufuatilia utekelezaji wa ahadi za nchi tajiri kuzisaidia nchi masikini kukabiliana na changamoto za afya za akina mama na watoto. Aidha, tunalo jukumu la kupendekeza mfumo wa kufuatilia jinsi fedha zinazotolewa, zinavyotumika kwa malengo yaliyokusudiwa. Tunatarajia kuanza kazi Januari 2011 na kuwasilisha Ripoti yetu kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kunako Mei 2011.

Michezo

Ndugu Wananchi;
Nafurahi kama tunavyofurahi wote kuwa kwa upande wa michezo, mwaka huu tumeumaliza vizuri. Timu ya Taifa ya Soka ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, imefanikiwa kushinda Kombe la Challenge kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati baada ya kufanya hivyo mara ya mwisho miaka 16 iliyopita yaani mwaka 1993.

Timu yetu ya Soka ya Wanawake, Twiga Stars, nayo kwa mara ya kwanza, iliweza kufikia fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake.

Hatuna budi kuyatambua na kuyaenzi mafanikio hayo tuliyoyapata. Wakati huo huo tuwatake wanamichezo wetu kuwa na ari ya kufanya vizuri zaidi. Nimetoa changamoto kwa TFF na timu yetu ya taifa kujiwekea lengo la kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2012. Wakiamua hivyo, itabidi waanze sasa kufikiria na kufanya maandalizi ya namna ya kufanikisha lengo hilo.

Napenda kutumia nafasi hii kuwahakikishia wanamichezo wote na Watanzania wenzangu, kuwa nitaendelea kuziunga mkono kwa hali na mali timu zetu zinazoshiriki michezo mbali mbali. Mwaka huu nitakuwa na mazungumzo na viongozi wa riadha ili tuelewane kuhusu namna ya kufufua michezo hiyo ambayo miaka ya nyuma ilililetea taifa letu sifa kubwa.

Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru

Ndugu Wananchi;
Mwaka mpya tunaouanza usiku wa leo una umuhimu wa kipekee katika uhai na historia ya nchi yetu. Tarehe 9 Desemba 2011 nchi yetu itatimiza miaka hamsini ya Uhuru wa Tanzania Bara. Haya si mafanikio madogo hata kidogo. Ni mafanikio makubwa sana ambayo hatuna budi kuyafurahia na kuyasherekea kwa uzito unaostahili.

Katika miaka 50 ya Uhuru wetu tumefanya mambo mengi mazuri ya kujivunia katika nyanja mbalimbali. Tumedumisha uhuru na umoja wa nchi yetu. Kwa hakika hali yetu ilivyo leo kisiasa, kiutamaduni, kiuchumi, kijamii, kiusalama na kimaendeleo kwa jumla, ni tofauti sana na hali ilivyokuwa wakati Tanzania Bara inapata uhuru wake tarehe 9 Desemba, 1961. Natambua pia kwamba katika miaka 50 hii, nchi yetu na watu wake wamekumbana na kukabili changamoto nyingi. Zipo nyingi tulizoziweza na zipo ambazo tunaendelea kuzikabili na tunayo mipango thabiti ya kuhakikisha tunafanikiwa.

Ndugu Wananchi;

Kwa kutambua umuhimu wa aina yake wa maadhimisho ya mwaka huu ya siku ya Uhuru wa Tanzania Bara tarehe 9 Desemba, 2011, tumekubaliana na viongozi wenzangu Serikalini kuwa tusherehekee siku hiyo kwa uzito unaostahili.

Ndugu Wananchi;

Tumekubaliana pia, tufanye mambo manne muhimu katika maadhimisho hayo. Kwanza, nautangaza mwaka 2011 kuwa ni Mwaka wa Maadhimisho ya Miaka Hamsini ya Uhuru wa Tanzania Bara. Kilele chake kitakuwa tarehe 9 Desemba, 2011 ambapo kutafanyika sherehe kubwa na za aina yake nchi nzima ambapo wananchi watashirikishwa kwa ukamilifu.

Pili, tufanye tathmini ya kina ya mafanikio tuliyoyapata, katika juhudi zetu za kujiletea maendeleo katika miaka hamsini hii. Kila Wizara, idara na taasisi za Serikali na hata sekta binafsi zifanye tathmini ya eneo lake. Tathmini hizo ziandikwe katika vitabu ili kuhifadhi kumbukumbu hizo muhimu kwetu na kwa vizazi vijavyo. Vitabu na nyaraka hizo vitakuwa kumbukumbu zenye manufaa makubwa kwa wenzetu watakaokuwepo mwaka 2061 wakati wa kusherehekea miaka 100 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Itarahisisha kazi yao ya kufanya tathmini wakati huo.

Tatu, kwamba yafanyike maonyesho maalum katika Uwanja wa Maonyesho wa Julius Nyerere hapa Dar es Salaam na kote mikoani kwenye viwanja vya maonyesho, kuelezea mafanikio yaliyopatikana katika nyanja mbalimbali katika miaka 50 tangu Uhuru wa Tanzania Bara.

Ndugu Wananchi;

Jambo la nne ambalo tulilokubaliana kufanya ni kuanzisha mchakato wa kuitazama upya Katiba ya Nchi yetu kwa lengo la kuihuisha ili hatimaye tuwe na Katiba inayoendana na taifa lenye umri wa nusu karne. Katiba yetu ya sasa tuliyoachiwa na waasisi wa taifa letu, imeifanyia nchi yetu mambo mengi mazuri na kuifikisha Tanzania na Watanzania hapa tulipo. Tunayo nchi moja huru, ya kidemokrasia na inayoendesha mambo yake kwa kuzingatia utawala wa sheria, kuheshimu haki za binadamu na mgawanyo wa madaraka miongoni mwa mihimili mikuu ya dola. Nchi yenye amani, utulivu na watu wake ni wamoja, wanaopendana na kushirikiana na maendeleo yanazidi kupatikana.

Pamoja na hayo, mwaka 2011, nchi yetu inatimiza miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, miaka 47 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar na miaka 47 ya Muungano wa nchi zetu mbili. Yapo mabadiliko mengi yaliyotokea katika nyanja mbalimbali za maisha ya nchi yetu na watu wake katika kipindi hiki. Kwa ajili hiyo ni vyema kuwa na Katiba inayoendana na mabadiliko na matakwa na hali ya sasa. Katiba ambayo italipeleka taifa letu miaka 50 ijayo kwa salama, amani, umoja na kuwepo maendeleo makubwa zaidi.


Ndugu Wananchi;

Ndiyo maana tukaamua kuanzisha mchakato huu na kwa ajili hiyo, nimeamua kuunda Tume maalum ya Katiba, yaani Constitutional Review Commission. Tume hiyo itakayoongozwa na Mwanasheria aliyebobea, itakuwa na wajumbe wanaowakilisha makundi mbalimbali katika jamii yetu kutoka pande zetu mbili za Muungano. Jukumu la msingi la Tume hiyo litakuwa ni kuongoza na kuratibu mchakato utakaowashirikisha wananchi wote bila kubagua, vyama vya siasa, wanasiasa, wafanyabiashara, asasi za kiraia, mashirika ya dini, wanataaluma na makundi mbalimbali ya watu wa nchi yetu kote nchini, katika kutoa maoni yao juu ya wayatakayo kuhusu Katiba ya nchi yao.

Baada ya kukamilisha kukusanya maoni, Tume itatoa mapendekezo yake yatakayofikishwa kwenye vyombo stahiki vya Kikatiba kwa kufanyiwa maamuzi. Baada ya makubaliano kufikiwa, taifa letu litapata Katiba mpya kwa siku itakayoamuliwa ianze kutumika.

Ndugu Wananchi;

Ni matumaini yangu kuwa mchakato huo utaendeshwa vizuri, kwa amani na utulivu kama ilivyo sifa ya nchi yetu na mazoea yetu ya kujadiliana bila kugombana. Wananchi watapewa fursa ya kutosha ya kutoa maoni yao kwa uhuru na pawepo kuvumiliana kwa hali ya juu pale watu wanapotufautiana kwa mawazo. Pasiwepo kutukanana, kudharauliana, kushutumiana, kubezana, kuzomeana wala kushinikizana. Naomba washiriki waongozwe kwa hoja badala ya jazba. Tukiwa na jazba, hasira na kushinikizana kamwe hatutaweza kutengeneza jambo jema. Na inapohusu Katiba ya Nchi itakuwa hasara tupu. Haitakuwa endelevu na kulazimika kufanyiwa marekebisho mengi mwanzoni tu baada ya kutungwa.

Nawaomba Watanzania wenzangu wenye maoni yao wajiandae kushiriki kwa ukamilifu katika mchakato huu. Katoeni maoni yenu mazuri yatakayowezesha nchi yetu kuwa na Katiba itakayokidhi matakwa yetu ya sasa na ya miaka 50 ijayo.

Hitimisho

Ndugu Wananchi, Watanzania Wenzangu;
Napenda kumalizia salamu zangu za Mwaka mpya kwa kumshukuru tena Mwenyezi Mungu kwa rehema zake alizotujaalia mwaka 2010. Tuendelee kumuomba atujaalie baraka tele katika Mwaka ujao wa 2011: Tumuombe nchi yetu iendelee kuwa ya amani na utulivu, watu wake waendelee kuwa wamoja, wanaopenda na kushirikiana, uchumi wetu uendelee kustawi, tupate mvua za kutosha na neema ziwe tele kila mahali.

Kwa furaha na matumaini makubwa nawatakia heri na fanaka katika mwaka mpya 2011. Namtakia kila mmoja wetu mafanikio mema katika shughuli zake za kujiletea maendeleo na kuendeleza hali yake ya maisha.
Mwisho, kabisa nawaomba tuukaribishe na kuusherehekea Mwaka mpya kwa usalama na amani. Heri ya Mwaka Mpya!! Happy New Year!!

Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Ahsanteni kwa kunisikiliza.

(Video ya hotuba hii inaandaliwa)
Rais Jakaya Kkwete amemteua Dkt. Mwelecele Malecela (pichani) kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Magonjwa ya Binadamu (NIMR). Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa leo na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, uteuzi huo unaanza Desemba 14, 2010.
Dkt. Malecela ana shahada ya juu ya uzamivu ya vimelea vya magonjwa ya binadamu katika fani ya matende na mabusha kutoka chuo kikuu cha London University, Uingereza. Amefanya kazi NIMR kwa miaka 23 sasa na kushika nyadhifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mkurugenzi na Uratibu na Kukuza utafiti, na amekaimu nafasi ya Mkurugenzi mkuu Nimri toka mwaka 2009
Ali Fereji Tamim


Ali Fereji Tamim amefanikiwa kutetea kiti chake cha Urais wa Chama cha soka cha Zanzibar (ZFA) baada ya kupata kura 32 kati ya 54 zilizopigwa katika uchaguzi mkuu wa chama hicho uliofanyika leo huko Pemba.

Tamima amemshinda mpinzani wake wa karibu Suleiman Jabir aliyepata kura 20 wakati mgombea mwingine wa nafasi hiyo Munir Zakaria kambulia kura mbili.

Nafasi ya Makamu wa Rais imeenda kwa Amani Makungu aliyejipatia kura 32, akimshindaga Haji Ameir ambaye alijikuta anakiacha kiti hicho baada ya kupata kura 22.

Nafasi ya Makamu wa Rais kwa Pemba imechukuliwa na Ali Mohamed
Ali ambaye alichota kura 44, baada ya aliekua anashikilia nafasi hiyo Suleiman Amour kujitoa.
Fuvu la kichwa la marehemu Martine Kiyeyeu mkazi wa kijiji cha Mlolo kata ya Mseke wilaya ya Iringa vijijini likitolewa kaburini
Mabaki ya mwili wa Kiyeyeu yakiwekwa katika jeneza tayari kwa kwenda kuzikwa upya baada ya eneo la awali kuchimbwa kaburi lake ili kupisha upanuzi wa barabara kuu ya Iringa -Mbeya
Jumla ya makaburi nane ndio ambayo yameondolewa katika eneo hilo na hakuna tukio lolote la ajabu lililopata kujitokeza pamoja na kuwepo kwa maneno mengi toka eneo hilo. Picha na mdau Francis Godwin.

Ankal alitembelea eneo hili mwezi wa Septemba,
kabla ya makaburi kuhamishwa.
BOFYA HAPA




The Kilimanjaro Band 'Wana Njenje' (pichani) wataukaribisha mwaka mpya leo katika kiota chao cha kila siku cha Salender Bridge Club jijini Dar, na kesho pia wataendelea na 'Kinyaunyau' katika kuadhimisha mwaka 2011. Kwa mujibu wa kiongozi wa bendi hiyo kongwe, Waziri Ally, Njenje imebidi waduarike mkesha wa mwaka mpya na kuendelea na libeneke kesho kutokana na maombi ya wapenzi wa muziki wa kistaarabu

no image
Blogu yako ya jamii, Chachandu Daily, imekuwa ikikupa habari za kweli na za muhimu katika nyanja mbalimbali kwa wakati mwafaka katika kipindi chote cha mwaka 2010. Na sasa inakuahidi kuwa katika mwaka wa 2011 pia itakuwa nawe bega kwa bega, mguu kwa mguu au chochote kwa chochote kuhakikisha inakufikishia karibu na habari moto moto kwa wakati na wepesi.
Endelea kuperuzi blogu hii na kutoa maoni yako bila kuchoka kwani ipo kwa ajili yako wewe na mwenzako. Nakutakia/nawatakia heri ya kweli ya mwaka mpya wa 2011, uwe wa kheri, fanaka na wenye neema na afya njema kwa kila rika na jinsia. Kuperuzi Bofya Link hii:-
www.bashir-nkoromo.blogspot.com
no image
A Michigan man who says he learned of his wife's infidelity by reading her e-mail faces felony charges of computer misuse.

Prosecutors, relying on a Michigan statute typically used to prosecute crimes such as identity theft or stealing trade secrets, have charged Leon Walker, 33, with a felony after he logged onto a laptop in the home he shared with his wife, Clara Walker. If convicted in the trial that begins Feb. 7, he could be sentenced to five years in prison.

Using her password, he accessed his wife's Gmail account and learned she was having an affair. She filed for divorce, which was finalized this month.

Leon Walker told the Oakland Press of Pontiac, Mich., that he was trying to protect the couple's children from neglect. He called the case a "miscarriage of justice."

Oakland prosecutors say the charge is justified.
Mshindi wa kwanza kwa upande wa wanaume kwa kilometre 21 Vodacom babati half Marathon ndugu Fabian Joseph akipokea kikombe kutoka kwa mgeni rasmi mh. Claudio Bitegeko Regional Admistrative Secretary wa mkoa wa Manyara.Washiriki wa mashindano ya Vodacom babati half marathon wakiwa tayari kwa kuanza mashindano katika ofisi za Manyara internet café.




Burudani zilikuwepo
Mshindi wa kwanza wa Vodacom babati half
marathon (km 21) ndugu Fabiani Joseph akiingia kwenye uwanja wa babati. Washindi walikuwa kama ifuatavyo
Wanaume:-
Fabian Joseph
Dickson Marwa
Msenduki Mohamed
Ezekia Japhari
Ismail Juma

Wanawake:-
Restituta Joseph
Zakia Mrisho
Jackline sakilu
Zaituni Jumanne
Catherine Irangi.



Mwenyekiti wa bodi ya Benki ya KCB Tanzania Dr.Edmund Mndolwa(kushoto) akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Hai Dr.Norman Sigalla mfano wa hundi ya shilingi Milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya Sekondari ya Lyasikika ya wilayani humo. Wa pili toka kushoto ni Mkurugenzi wa masoko na uhusiano wa benki hiyo Christina Manyenye,Mkuu wa kitengo cha mikopo Ronald Kitti. Hafla hii ilifanyika katika makao makuu ya Benki hiyo jijini Dares Salaam leo.

Kuna mwamko mkubwa sana wa wananchi kutumia huduma mbalimbali za benki badala ya kuweka pesa mchagoni. raha ni pale inapokuja swala la kuchukua ngawira hasa kwa ATM. Foleni ni za kufa mtu na inatoa changamoto kwa mabenki sio tu kuongeza huduma hii bali pia kusambaza mashine hizo kwa wingi kila sehemu ili kupunguza ama kuondoa kabisa raha hii
no image
Ndugu Michuzi.

Kwa niaba ya kanisa zima la Umoja,ninapenda kuwakaribisha watanzania wote na watu kutoka mataifa mbali mbali ya Afrika katika ibada ya kwanza ya mwaka wa 2011.

Ibada hii maalumu ya kuanza mwaka itaanza saa kumi na moja na nusu mpaka saa moja na nusu jioni (5:30pm-7:30pm).Katika ibada hii mchungaji Absalom Nasuwa atakuletea ujumbe maalumu wa neno la Mungu utakaokuongoza katika mwaka mzima wa 2011.

Maombi mbali mbali yatafamywa kwa kila moja wetu kama silaha ya kukulinda na hila mbali mbali za shetani. Kumbuka "Yesu Kristo ni yeye yule jana na leo na hata milele"
Kwa mawasiliano zaidi tupigie kwa namba hizi:

214 554 7381, 682 552 6402, 214 773 6697

Mahali:
Kanisa la Umoja International Outreach;
6411 LBJ FREEWAY
DALLAS TX,75240

Mungu awabariki na karibuni wote

Umoja Church.
no image
KAMPUNI KUBWA YA ULINZI ZANZIBAR INATANGAZA NAFASI KADHAA ZA KAZI YA ULINZI.

SIFA ZA MWOMBAJI
1. Awe Mtanzania mwenye cheti cha kuzaliwa au affidavit.
2. Awe na elimu ya msingi au sekondari.
3. Awe amepitia mafunzo ya JKT au Mgambo.
4. Awe na umri baina ya miaka 23 hadi 35
5. Urefu zaidi ya futi 5 itkuwa nzuri zaidi.

Kwa nafasi za Supervisors, mwombaji atatakiwa awe na uwezo wa kuandika na kuzungumza kiingereza pamoja na sifa hizo hapo juu.

SEHEMU YA KUFANYIA KAZI ITAKUWA ZANZIBAR TU.
Mwombaji atatakiwa kuwa na makazi kwa muda wa wiki 3 za mafunzo na baada ya hapo anaweza kubahatika kupata makazi bure.

Kwa maelezo zaidi, piga simu namba 0767 237 168

Tafadhali mwambie mwenzio habari hizi.
Marehemu Mary John Mwingira.


The Family of the late John & Mary Mwingira of Upanga and Kunduchi, Dar Es Salaam

wish to extend sincere appreciation for your exceptional kind of sympathy during the time of great pain and loss of our beloved mother

Mary John Mwingira

who was recalled to the Lord on 21st November 2010.

It was so comforting to see you standing beside us.

Your presence, actions and kind words touched us deeply.

We are sincerely grateful for all the generous, moral and material support that you provided to us.

Thank you for attending her funeral, it meant so much to us

A memorial Eve will be held on Friday 31/12/2010 at Dr. Ndalama’s Residence, Kunduchi beach (madini)

followed by a Mass which will be held on Saturday, 1st January 2011, 1000hrs at the same venue.

You are all welcome.

To you Loving Mama: Words cannot express the pain we have! Its such a great loss to us all your Children, Grandchildren, workmates, Relatives and Friends from different corners of this living world. We promise Mama to live your legacy. You are such a great woman in this this family, nation and the world.

Rest In Peace Mama!!!

************************************

Ratiba ya Maadhimisho ya Kumbukumbu ya

Marehemu Mary John Mwingira

31st December 2010; Ijumaa

1700hrs: Kinondoni Makaburini

1. Kujengea Msalaba kwenye Kaburi la Marehemu
2. Sala ya kumuombea Marehemu

1800hrs: Ndugu, jamaa na marafiki kuelekea Nyumbani Kunduchi Beach (Kwa Dr. Ndalama) kuendelea na ratiba ya Mkesha

2000hrs: Chakula cha usiku

2030hrs na Kuendelea: Sala pamoja na Nyimbo za maombolezo

1st January 2011 [ Nyumbani - Kunduchi Beach]

0700hrs: Kifungua kinywa

1000hrs: Misa Takatifu (itafanyikia nyumbani, Kunduchi beach)

1230hrs: Chakula cha mchana

TULIMPENDA,LAKINI MUNGU ALIMPENDA ZAIDI.
JINA LA BWANA LIHIMIDIWE.

-AMIN
no image

Ndugu Ankal!

Tunashukuru kwa kuweka kwenye mtandao wetu huu wa jamii ile jumatatu Kero ya jinsi uchafu ulivyokuwa umeachwa majumbani kwetu Sinza kwa zaidi ya mwezi na wiki kadhaa. Hatimae, nadhani wahusika walisikia kilio chetu kwa kupitia Globu hii ya Jamii. Jana matakataka yamezolewa na saa hizi tunafurahi kuwa tunaingia mwaka mpya na harufu safi. Tunaomba adhabu ya kuachiwa matakata isirudie tena kwa mwaka huu mpya wa 2011.

Tunamshukuru Mungu kero hii imetoka na tunaomba isirudie tena. Nadhani kuna uongozi wa juu uliliona hili na wahusika wakalifanyia kazi. Katika maoni kulikuwa na malumbano makubwa ,lakini yote yalilenga katika kujenga na sio kubomoa.

Wana Sinza kwa Wajanja Hoyeee!!! Mungu atubariki sote tuanze mwaka mpya 2011 kwa furaha na Shange na Mafanikio mengi. Harufu Mbaya MWIKO!

Libeneke Oye!

no image
Nahitaji msaada wa kukutanishwa na mtu anaeweza kufundisha kidutch au kama kuna darasa la kidutch hapa Dar kama kuna community ya wadutch au watu wanaojua kidutch kwa ajili ya kupractise na kufundishwa pia.
mdau Shella

Celebrating Bongo Films, Bongo Sounds, Music and Performances!

From Friday 31st Dec 2010 to 2nd January 2011

Friday 31st Dec. Shows:

Films on the Big Screen:

This is it –Star: Steven Kanumba, Hanifa Daudi, Othman Njaidi,

Huba – Star: Ahmed Olutu, Natasha & Hashim Kambi,

Saturday 1st Jan Show:

Films on the Big Screen:

Don’t Cry – Star: Haji Adam

Divorce–Star:Vincent Kigosi,

Sunday 2nd Jan Show:

Films on the Big Screen:

Awards Night-Winning Film

Followed by:

Performances by: Tanzania House of Talents (THT)

Mwasiti, Marlaw, Mataluma, Amini, Barnabas, Ditto, Lina, THT Band and Dancers

Ticket Price:

Tsh 5000/- Local & Tsh 10,000/- Foreigner

In the Old Fort (Ngome Kongwe) from 7pm to 1am

Mhariri Mkuu wa Jambo Leo, Boniface Wambura (wa pili kushoto),ambaye ameteuliwa kuwa Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), akikabidhiwa zawadi ya kompyuta ndogo iliyotolewa na uongozi wa Kampuni ya Jambo Concepts Tanzania Limited (JCTL), wakati wa hafla ya kumuaga Dar es Salaam jana. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa JCTL, Juma Pinto, Meneja Mkuu, Ramadhani Kibanike, Mkurugenzi, Benny Kisaka na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Perfect Solutions, Evance Aveva ambaye ni Mshauri wa JCTL.
Mkurugenzi Mkuu wa JCTL, Juma Pinto akitoa
nasaha wakati wa hafla hiyo.

Mkurugenzi wa JCTL, Benny Kisaka akitoa
nasaha wakati wa hafla hiyo.

I am Lulu Mero a Tanzanian girl. Wrote this book in two languages; English and Kiswahili. It is an interesting book, you are encouraged to read in your life time. The title takes over my philosophy of flotation. Which are; Life is all about floating because there is wavy, calm and deep water and God is our water surround. Thanks/Ahsante~
For More
CLICK HERE
Mdau Bachalla akiwa na Bob Farell jijini Amsterdam
BOFYA HAPA

Na mdau Ughaibuni

Bobby Farrell (61) ambaye alikuwa mwanamziki mashuhuri katika miaka ya 1970s kutoka kundi maarufu enzi hizo Boney M, Mr.Bobby Farrell amekutwa amefariki dunia katika chumba cha hotel aliyofikia mjini St.Petersburg,nchini Urusi.

Mwanamziki huyo alikuwa katika ziara ya kimziki nchini urusi,maiti yake iligunduliwa katika chumba cha hotel aliyofikia baada ya kumaliza show zake.idara ya usalama ya mji wa St.Petersburg umeunda kamati maalumu kuchunguza chanzo
cha kifo cha Bobby farrell.

Marehem Bobby Farrell (61) alikuwa mwanamziki anayeongoza safu ya mbele ya iliyokuwa bendi maarufu duniani Boney M,ambapo alifanyakazi na wanamziki Maisie Williams,Liz Mitchel na Marcia Barret.

Kundi la Boney M lilijizolea umaarufu kila kona duniani kutokana na umahili wa nyimbo zake kutingisha katika madisco na redio za kimataifa, Kundi hilo lilikuwa na maskani yake nchini Ujerumani na kuweza kupiga tour katika kila kona duniani.

Baada ya kundi la Boney M kusambaratika marehem Bobby Farrell alihamishia makazi mjini Amsterdam,nchini uholanzi.