Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewatoa hofu na kuwahakikishia wananchi, wasafiri na wasafirishaji kuwa ameweka kambi Mkoa wa Lindi kuhakikisha anasimamia timu ya watalaamu wa Wakala ya Barabara (TANROADS) na makandarasi, kuhakikisha wanakamilisha kazi ya kurejesha mawasiliano ya barabara ya Lindi – Dar es Salaam ndani ya saa 72.

Waziri Bashungwa ameeleza hayo, leo tarehe 6 Mei 2024 Nangurukuru Wilayani Kilwa wakati akikagua na kusimamia zoezi la urejeshaji wa mawasiliano ya barabara yaliyokatika kwa kuharibiwa na mvua kubwa zilizonyesha zikiambatana na kimbunga Hidaya.

“Niendelee kuwatoa hofu wananchi na wasafiri wanaotumia barabara hii inayounganisha mikoa ya kusini, tangu jana nimepiga kambi huku, nilianzia Somanga na sasa hivi tupo upande huu wa Nangurukuru, kama mnavyoona pande zote wanaendelea na kazi, bado tunaamini ndani ya saa 72, kufikia Alhamisi tutakuwa tumekamilisha kazi ya kurudisha mawasiliano ya barabara hii,” amesema Bashungwa.

Bashungwa amemuagiza Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Mohamed Besta kuhakikisha anaongeza idadi ya malori yanayosomba mawe pamoja na mitambo inayotumika kupakia mawe katika magari ili kuongeza kasi ya kujaza vifusi katika eneo la barabara yaliyosombwa na maji.

Aidha, Bashungwa amesema kuwa pamoja na jitihada za kuagiza makalvati ya plastiki yanayotumika katika dharura za kurejesha mawasiliano ya barabara, ameeleza kuwa ili kukamilisha kazi hiyo kwa wakati watalazimika kutumia makontena kwa kuyakata yatumike kama mbadala wa kalvati na kuwezesha maji kupita.

Kadhalika, Bashungwa amewapongeza wahandisi kutoka TANROADS pamoja na makandarasi wote wanaoendelea na kazi ya kuhakikisha mawasiliano ya barabara katika maeneo yote yaliyokatika yanarejea.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mohamed Nyundo amemshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha Mamlaka ya Hali ya Hewa kuwa na vifaa vya kisasa vinavyotumika kutabiri hali ya hewa ambapo vimesaidia kwa kiasi kikubwa kutoa utabiri wa matukio mbalimbali ikiwa ni pamoja na mafuriko makubwa na kimbunga Hidaya.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kivinje Singino, Jafari Bakari ameipongeza Serikali kwa kuchukua hatua za haraka na dharura kwa kufanyia kazi changamoto zinazojitokeza ikiwa ni pamoja na kuhamisha wananchi wanaokaa katika maeneo hatarishi.

Muonekano wa sehemu ya barabara ya Lindi - Dar es Salaam, eneo la Nanguruku ambalo limekatika kutokana na Mvua kubwa zilizonyesha zikiambatana na Kimbunga Hidaya, Mkoani Lindi.

Muonekano wa mitambo na magari yakiwa katika zoezi la urejeshaji wa miundombinu ya barabara ya Lindi – Dar es Salaam, eneo la Nanguruku ambalo limekatika kutokana na Mvua kubwa zilizonyesha zikiambatana na Kimbunga Hidaya, Mkoani Lindi.

 


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akitoa maelekezo kwa Msimamizi wa Matengenezo kutoka Wakala ya Barabara (TANROADS), Mkoa wa Lindi, Eng. Robert Mosea wakati akikagua na kusimamia zoezi la urejeshaji wa mawasiliano ya barabara ya Lindi – Dar es Salaam yaliyokatika kwa kuharibiwa na mvua kubwa zilizonyesha zikiambatana na kimbunga Hidaya, Mkoani Lindi.



RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan ameagiza huduma za dharura zipelekwe kwenye maeneo yaliyopata athari kutokana na kimbunga Hidaya.

Hayo yamesemwa leo (Mei 6, 2024) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwenye kikao cha dharura cha Kamati ya Maafa Kitaifa alichokiitisha kupokea taarifa ya hatua zilizochukuliwa kwenye maeneo yaliyopata athari.

“Rais ameelekeza hatua za haraka zichukuliwe katika maeneo yote yaliyoathiriwa na mvua zilizotokana na athari za kimbunga Hidaya ikiwa ni pamoja na kupeleka misaada,” amesema. Maeneo yatakayopelekewa misaada hiyo ni Mafia mkoani Pwani, Kilwa (Lindi) na Ifakara (Morogoro).

Waziri Mkuu ameliagiza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lihakikishe linakamilisha zoezi la uokoaji katika maeneo ya Kilwa ambapo zaidi ya kaya 40 zimezingirwa na maji. “Jeshi la Zimamoto mmefanya kazi kubwa, hakikisheni maeneo yenye makazi yaliyozingirwa na maji, wakazi wake wanaondolewa na kupelekwa maeneo salama pamoja na kupewa huduma zote muhimu.”

Wakati huohuo, Waziri Mkuu ameziagiza Wizara za Ujenzi, Uchukuzi, Afya, Maji, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mambo ya Ndani ya Nchi, Ulinzi na Fedha zichukue hatua za dharura ili kuhakikisha hakuna madhara zaidi yanatokea katika maeneo yaliyopatwa na athari.

“Wizara ya Ujenzi endeleeni kuchukua hatua zote za dharura zinazohitajika kuhakikisha maeneo ya barabara yaliyokatika yanarekebishwa na huduma za usafiri zinarudi haraka.”

Waziri Mkuu amepongeza jitihada zinazofanywa na Idara ya Menejimenti ya Maafa kwa kuendelea kufanya uratibu katika maeneo yote yaliyoathirika na kuwataka waendelee na uratibu katika maeneo yaliyopata madhara kuanzia juzi.

“Ongezeni nguvu katika maeneo ya Ifakara, Kilwa na Mafia na kuhakikisha wananchi wote walioathiriwa wanakuwa katika maeneo salama na wanapata huduma zote za msingi za kijamii.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameiagiza Kamati ya Maafa ya Kitaifa izisimamie Kamati za mikoa na Wilaya ili misaada inayotolewa kwa waathirika iwafikie walengwa. “Kamati ya Kitaifa izielekeze Kamati za Mikoa na Wilaya zisimamie misaada yote ya waathirika ili ifike kwa wahusika, baadaye hali ikisharejea, tutataka tupate taarifa ya kina na jinsi ilivyotumika,” amesisitiza.

Na Jane Edward, Arusha

Sheikh Hussein Said Junje, Sheikh wa Wilaya ya Arusha Mjini amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumteua Mhe. Paul Christian Makonda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha akimsifu kwa Uwajibikaji wake katika kusimamia haki za wananchi wa Arusha.

Sheikh Junje ametoa kauli hiyo Ofisini kwake Mjini Arusha wakati akizungumzia programu maalum ya Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Arusha ya kutenga siku tatu Maalum za kusikiliza na Kutatua kero za wananchi ambazo zitakuwa Jumatano, alhamisi na Ijumaa ya Wiki hii.

Sheikh Junje amemtaja Mhe.Mkuu wa Mkoa Paul Christian Makonda kama kiongozi mwenye kuzingatia Kanuni zinazotokana na Quran na Sunnah za Mtume (SAW) ambazo ni Haki, Mashauriano, wajibu, Unyenyekevu na Huruma, akisema anayoyafanya Mhe. Mkuu wa Mkoa yanampendeza Muumba wetu aliyeumba pia Mbingu na Ardhi.

Ikumbukwe kuwa Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Christian Makonda amewaalika wananchi wote wa Arusha wenye changamoto na kero mbalimbali kufika ofisini kwake tarehe 8-10 Mei, 2024 ili kuweza kusikilizwa na kutatuliwa changmoto walizonazo huku Mkuu wa Mkoa akiahidi kujiandaa vya kutosha yeye na wasaidizi wake ili kuweza kuhakikisha wananchi wanapata haki zao kama yalivyo Maelekezo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Kamati ya Baraza la Wawakilishi ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati Zanzibar, imefanya ziara kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ili kupata uzoefu wa shughuli za udhibiti leo tar. 6 Mei 2024.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Yahaya Rashid Abdala, ameishukuru EWURA kwa kuwakaribisha vizuri na kueleza imani yake kuwa watajifunza masuala mengi muhimu kuhusu udhibiti.

Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andilile, alisema EWURA ipo tayari wakati wote kutoa mafunzo na taarifa za masuala ya udhibiti kwa wadau mbalimbali nchini.

“Napenda kuwakaribisha sana EWURA, tumefarijika kwa ujio wenu, tutawapa ushirikiano wa hali ya juu ili lengo la ziara hii lifikiwe” Alisema.

Mada zitakazowasilishwa katika mafunzo hayo ni pamoja na majukumu na wajibu wa EWURA, Udhibiti wa mafuta, udhibiti wa gesi asilia, udhibiti wa sekta ya umeme, udhibiti wa majisafi na usafi wa mazingira, sheria na kanuni pamoja na masuala ya bei.

Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt James Andilile ( aliyesimama) akiwakaribisha wajumbe wa Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar walioitembelea EWURA kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya udhibiti.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe Yahya Rashid Abdala, akiwaongoza wajumbe wakati wa mafunzo ya masuala ya udhibiti katika Ofisi za EWURA makao makuu jijini Dodoma.

Watendaji wa EWURA wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Dkt James Andilile( kulia) wakati wa semina kuhusu udhibiti wa huduma za nishati na maji kwa Wajumbe wa Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar iliyofayika makao makuu ya EWURA.

Wajumbe wa Kamati ya Mawasiliano Ardhi na Nishati wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wakiendelea na semina kuhusu masuala ya udhibiti katika ofisi za EWURA Makao Makuu jijini Dodoma..

 
Dar es Salaam. Tarehe 6 Mei 2024: Benki ya CRDB imeandika historia nyingine kwa kupokea cheti cha kimataifa cha masuala ya mazingira baada ya jengo lake la Makao Makuu kukidhi vigezo vya kimataifa vya majengo yenye kuzingatia uhifadhi wa mazingira.

Cheti hicho cha kwanza kutolewa kwa majengo ya hapa nchini, kinatolewa na taasisi ya International Finance Corporation (IFC) ambayo ni kampuni tanzu ya Benki ya Dunia chini ya programu yake ya EDGE (Excellence in Design for Greater Efficiencies).

Akikabidhi tuzo hiyo, Mkuu wa Idara ya Majengo Yanayolinda Mazingira wa IFC, Dennis Quansah amesema ulinzi wa mazingira ni jukumu la kila mmoja na ni muhimu kuangalia kila kitu kinachochangia uchafuzi wa mazingira yanayoleta mabadiliko ya tabianchi na athari nyingine kwa viumbe viishivyo duniani.
“Ni furaha kwa IFC kulithibitisha jengo lenu kwamba linatunza mazingira. Hili ni jengo la kwanza kwa Tanzania. Cheti hiki tunachowapa ni utambulisho kwa taassisi na mashirika ya kimataifa yanayohamasisha utunzaji wa mazingira. Matumizi ya maji, nishati na vifaa vya ujenzi ni kati ya vigezo muhimu vinavyotumika kulitathmini jengo kabla ya kulithibitisha,” amesema Quansah.

Mkuu huyo amesisitiza kwamba Benki ya CRDB imeweka mfano unaopaswa kuigwa na taasisi nyingine nchini ili kuyaboresha majengo yao na kuunga mkono juhudi za kulinda mazingira na kuifanya dunia kuwa sehemu salama ya kuishi. 

Cheti hicho ni uthibitisho wa juhudi za Benki ya CRDB sio tu yenyewe kulinda mazingira bali kuwezesha juhudi zinazofanywa na watu wengine kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa kwa kufadhili miradi yenye mrengo wa kulinda mazingira.
Sekta ya makazi ni kati ya maeneo yanayochangia uchafuzi wa mazingira kutokana na aina ya vifaa vinavyotumika kwenye ujenzi wa nyumba, matumizi ya maji pamoja na nishati.

Akipokea tuzo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema cheti hiki kinadhihirisha safari  waliyoianza miaka mingi iliyopita hata wakawa taasisi ya kwanza ya fedha ukanda wa kusini na mashariki mwa Afrika kutambuliwa na Mfuko wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (GCF) Novemba 2019.
“Kwa niaba ya menejimenti na wafanyakazi wa Benki ya CRDB, ninafurahi kupokea tuzo hii ya kulitambua jengo letu la makao makuu kwamba linatunza mazingira tukikidhi vigezo kwenye vipengele vyote vitatu vinavyozingatiwa na IFC kabla ya kutoa cheti. 
 
Tumepunguza matumizi ya nishati kwa asilimia 21 na matumizi ya maji kwa asilimia 27. Vifaa tulivyovitumia kwenye ujenzi navyo vinapunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa kwa asilimia 28 hivyo kutufanya kuwa juu ya kiwango cha chini kinachokubalika,” amesema Nsekela.

Akifafanua kuhusu vigezo hivyo, Mkuu wa Kitengo cha Programu Endelevu wa Benki ya CRDB, Ramla Msuya amesema katika jengo la Benki ya CRDB, taa huzima zenyewe kama hakuna mtu ofisini na maji hayatoki iwapo hakuna mtu anayetaka kuyatumia.
“Taa zinatakiwa ziwake tu iwapo kuna mtu anahitaji mwanga na maji iwe maliwatoni au jikoni, yatatoka iwapo yanahitajika. Huwezi kukuta maji yanamwagika kwa kigezo kwamba mtu kasahau kufunga bomba, hapa kwetu bomba linajifunga lenyewe kama hakuna anayelitumia, hizi ni sifa ambazo hazipo kwenye majengo mengi nchini. 
 
Vifaa vilivyotumika kweny eujenzi wa jengo hili ambalo Rais Samia Suluhu Hassan alilisifia wakati analizindua pia vinajali mazingira. Taka zote zinazokusanywa humu ndani zinarejelezwa, huwezi kuon ataka zimezagaa popote,” amefafanua Ramla.

Ili kuziwezesha taasisi na watu wengine wanaotaka kuyaboresha majengo yao yaendane na vigezo vya kimataifa vya kutunza mazingira, Nsekela amesema Benki ya CRDB inatoa mikopo inayoendana na malengo hayo.
“Tunao wabia zaidi ya 200 tunaoshirikiana nao kufanikisha uwezeshaji huu. Benki ya CRDB peke yake inaweza kukopesha mpaka dola milioni 107 za Marekani na ikishirikiana na GCF mkopo unafika dola milioni 250 na hakuna kikomo tukishirikiana na wabia wetu wengine. 
 
Tunafanya hivi ili Tanzania nayo iwe miongoni mwa mataifa yenye miradi inayolinda mazingira.  Mwaka jana tulitoa Hatifungai ya Kijani na kukusanya fedha nyingi kwa ajili ya miradi hii. Tunamkaribisha kila mwenye wazo au mradi wa kulinda mazingira,” amesema Nsekela.





 






Mjumbe kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Singida Ndg Ahmed Misanga ambae pia ni mratibu wa shughuli za wazazi ikungi ametoa Vifaa Vya ujenzi wa nyumba ya Mtumishi wa Jumuiya hiyo
Misanga Ametoa Vifaa hivyo alipo tembelea na kujionea maendelo ya ujenzi huo.

"Nimetoa vifaa hivii ikiwa ni muendelezo wa Michango yangu katika ujenzi wa nyumba ya Mtumishi wa wazazi wilayani ikungi leo nimeleta
Seruji , nondo , pesa ya ufundi kwa ajili ya kufunga lentha katika jengo hili" Misanga

" Pia tutaendelea kutoa michango yetu ili jengo hili liweze kukamilika kwa wakati na mtumishi aweze kuingia ndani,"

" Na tunamipogo wa kununua fenicha za ndani ili mtumishi akijaa aje na mabegi tu ili asipate tabu siku ya kuhama kama atakuwa amepata uhamisho wa kwenda mkoa mwingine,".
Huku katibu wa Jumuiya ya wazazi walaya ya ikungi Bi HAWA GIDABUDAYI ameshukuru Mjumbe kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Singida Ndg Ahmed Misanga kwa kujitowa kwake kwa ajili ya jumuiya hiyi kwa kutoa Vifaa vya ujenzi wa nyumba hiyo ya mtumishi.

" Kwani hili zoezi la kujenga nymba za watumishi ni agizo la kutoka makao makuu na sisi tumeadha kulitekeleza kwa vitondo na kwa sasa tupo hatua ya Kufunga Lentha paka ifikapo mwezi wakumi kila kitu kitakuwa kimekamilika na mtumishi ataingia ndani," Amesema

Huku mwenezi wa chama cha mapinduzi wilaya ikungi Ndugu .NASSORO ISSAH Amesema chama kinawajubu wa kusimamia jumya zake ili ziweze kutimiza malengo yake.

"Hizi nyumba zitasaidia sana watumishi wetu wanaokuja huku wilayani kwani akifika tu anasehemu ya kulala, namini atafnyakazi zake kwa utulivu na kwa umakini kwasababu anasehemu ya uhakuka ya kuishi,".

" Sasa mtumishi wa wilaya ya ikungi akae tayari kuhamia baadaa ya lentha tunakwenda kupaua na kumalizia nyumba hiyo, " Ameongeza








Zoezi la urejeshaji wa miundombinu ya barabara kuu ya Lindi - Dar es Salaam katika eneo la Somanga Mkoani Lindi ukiendelea ambapo timu ya wataalam kutoka Wakala wa Barabara (TANROADS) wanasimamia zoezi hilo kikamilifu ili kuruhusu mawasiliano kurejea kwa haraka.

Aprili 5,2024 Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa aliongea na wananchi waliokwama katika eneo hilo na kutoa taarifa yakuwa urejeshaji wa miundombinu ya barabara hiyo unatarajiwa kukamilika ndani ya saa 72 na kuweza kuruhusu magari na wananchi kupita katika eneo hilo.








Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi na kutaja  mafanikio ya Shirika la Uwakala  wa Meli Tanzania (TASAC).

Baadhi ya watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Uchukuzi ikiwemo TASAC  wakifatilia Bajeti ya Wizara hiyo.

Na Mwandishi Wetu ,Dodoma

WAZIRI wa Uchukuzi Prof. Makame M. Mbarawa (Mb.) amesema Serikali kupitia Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) imeendelea kutoa huduma za udhibiti wa huduma za bandari, usafiri majini na kutoa huduma ya biashara ya meli kwa bidhaa mahsusi  Tanzania Bara.

Akizungumza wakati wa kuwasilisha bungeni Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka wa Fedha 2024/25 Mhe. Mbarawa amesema TASAC imeendelea kusimamia watoa huduma za usafiri kwa njia ya maji kwa kufanya tathmini na kutoa leseni na vyeti vya usajili kwa watoa huduma waliokidhi vigezo.

“Serikali kupitia TASAC imeendelea kutoa leseni na vyeti vya usajili kwa watoa huduma waliokidhi vigezo. Hadi kufikia Machi, 2024 jumla ya watoa huduma 1,722 waliosajiliwa na kupewa leseni ikilinganishwa na jumla ya watoa huduma 1,498 katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2022/23 sawa na ongezeko la asilimia 14.95” amesema Mhe. Mbarawa.

Aidha ameongeza kuwa, katika kipindi cha kuanzia Julai, 2023 hadi Machi, 2024, Serikali kupitia TASAC imeendelea kurasimisha bandari bubu za Tanzania Bara ikiwa na lengo la kuimarisha  ulinzi na usalama katika maeneo ya bandari ili kuboresha utoaji wa huduma.

Aliongeza kuwa, jumla ya bandari bubu 99 zilikaguliwa na kufanyiwa tathmini ya kina na Serikali kupitia TASAC kwa kushirikishana na Mamlaka mbalimbali za  Serikali ambapo bandari 45 zilirasimishwa . 

Lengo la hatua hii ni kuhakikisha kuwa Serikali inaimarisha ulinzi na usalama katika maeneo ya bandari ili kuboresha utoaji wa huduma.

Kuhusu shughuli za utafutaji na uokoaji, Serikali kupitia TASAC imeendelea kuratibu shughuli hizo kupitia Vituo vya Utafutaji na Uokoaji Majini vilivyopo Dar es Salaam na Mwanza (Maritime Rescue and Coordination Centre – MRCC).

“Ili kuboresha usalama wa usafiri katika Ziwa Victoria, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Uganda chini ya uratibu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kupitia Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria zimeendelea kutekeleza Mradi wa Kikanda wa Kuboresha Mawasiliano na Uchukuzi Katika Ziwa Victoria wenye lengo la kuimarisha huduma za utafutaji na uokoaji katika Ziwa” amesema Mhe. Mbarawa.

Hadi kufikia Machi, 2024 ujenzi wa Kituo Kikuu cha Kikanda cha Uratibu wa Masuala ya Utafutaji na Uokoaji katika Ziwa Victoria (Regional Maritime Rescue Coordination Centre - RMRCC) umefikia asilimia 26. Aidha, ujenzi wa vituo vidogo vitatu (3) vya utafutaji na uokoaji unaendelea.

SERIKALI imesema imebuni miradi mbalimbali ya kimazingira inayosaidia jamii kuweza kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi katika maeneo mbalimbali nchini.


Pamoja na hatua hizo pia, imeendelea kuihimiza jamii kutumia nishati mbadala na majiko banifu ili kupungunguza kasi ya ukataji wa misitu ambayo husababisha uharibifu wa mazingira.


Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi wakati akijibu maswali bungeni kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo bungeni jijini Dodoma leo tarehe 06, 2024.


Akijibu swali la Mbunge wa Mwera Mhe. Zahor Mohammed Haji aliyetaka kujua mpango wa Serikali kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika kuwakinga wananchi na madhara yanayoweza kutokea, Mhe. Katambi amesema Serikali inatekeleza miradi ya upandaji miti, usambazaji wa maji safi kwa matumizi ya majumbani na mifugo na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji.


Ametaja ujenzi wa kuta katika maeneo ya fukwe za bahari yanayokabiliwa na mmomonyoko wa ardhi, ujenzi matuta na mabwawa kudhibiti mafuriko, kuwezesha jamii kubuni miradi mbadala ya kuongeza kipato na iliyo rafiki kwa mazingira pamoja na urejeshaji wa maeneo ya ardhi yaliyoharibika kuwa ni jitihada zingine za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.


Akiendelea kujibu swali hilo, Mhe. Katambi amesema Serikali imeandaa Mkakati wa Kitaifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (2021), Mpango Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022-2032) na Mchango wa Taifa katika Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (2021) ambayo ina mchango katika kukabiliana na changamoto hiyo.


Ameongeza kuwa Serikali inashirikiana kikamilifu na jumuiya ya kimataifa katika kubuni mikakati na hatua madhubuti za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika ngazi zote ikiwemo kuridhia Mkataba wa Umoja wa Mataifa Kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, Itifaki ya Kyoto na Makubaliano ya Paris.


Aidha, Naibu Waziri Katambi amesema Serikali inaendelea kuelimisha wananchi kuhusu madhara yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi ili waweze kuchukua tahadhari na kujilinda na maafa yanayosababishwa na changamoto hizo, ambapo uelimishaji hufanyika kabla ya maafa kutokea.


Waziri wa Ardhi. Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Slaa (wa pili kulia) akikata utepe kuzindua rasmi mradi wa nyumba kwa bei  nafuu wa Sky Royal Jijini Dar es Salaam. Wengine kutoka kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Coral Property Holding Co.Ltd  Zhou Tao, Mkurugenzi wa Ardhi wizarani, Upendo Matotola na Mkurugenzi Mkuu wa Hainan International Ltd Li Jun.
James Prevost akizungumza wakati wa kuzindua rasmi mradi wa nyumba kwa bei  nafuu wa Sky Royal Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi  Mtendaji wa Coral Property Holding Zhou Tao akizungumza wakati wa kuzindua rasmi mradi wa nyumba kwa bei  nafuu wa Sky Royal Jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu
KATIKA mpango unaolenga kuunga mkono juhudi serikali za kuhakikisha kunakuwepo na nyumba za makazi bei, kampuni ya ya RE/MAX na ile ya Coral Property zimezindua mradi wa nyumba mpya za bei nafuu wa Sky Royal, mtaa wa Morocco Jijini Dar es Salaam.

Hafla ya uzinduzi wa nyumba hito iliyohudhuriwa na viongozi na wadau mbalimbali katika sekta ya nyumba, ambapo pamoja na mambo mengine, uzinduzi huo ulionyesha dhamira ya dhati ya ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi unaolenga kuwapatia watu makazi ya bei nafuu na yenye ubora wa hali ya juu.

Akizindua mradi huo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Slaa, ameyapongeza makampuni hayo mawili kwa mpango huo ambao amesema umekuja wakati mufaka haswa ikitiliwa maanani ongezeko la uhitaji wa nyumba za makazi Jijini Dar es Salaam.

"Ujenzi wa nyumba za bei nafuu ni muhimu sana hapa nchini; uamuzi wa kampuni hizi mbili wa kujenga nyumba bora ni mfano bora w akuigwa na taasisi nyingine hapa nchini ili kukabiliana na changamoto inayohusiana na mahitjai ya nyumba bora za makazi”, amesema.

Waziri Silaa aliendelea kusema kuwa, hatua zilizochukuliwa na makampuni hayo mawili zinaunga mkono juhudi za Serikali zinazolenga kuwepo kwa nyumba bora za makazi na za gharama nafuu kwa wananchi hapa nchini.

"Nichukue fursa hii kutoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa hii ya nyumba nzuri za makazi; ni matumaini yangu kuwa uwekezaji wa nyumba nzuri za makazi katika soko kutaiwezesha Serikali kufikia azma yake ya wananchi kuwa na nyumba nchini”, amesema.

Aidha Waziri Silaa ametoa wito kwa makampuni ya RE/MAX Coastal na Coral Property kujiongeza na kupanua panua wigo wa uwekezji wao kwa kuwekeza maeneo mengine hapa nchini ikiwemo Jijini Dodoma ambapo amesema idadi ya watu inakuwa ikongezeka kila siku na hivyo kusababisha ongezeko la mahitaji ya nyumba za makazi na zenye gharama nafuu.

Tukio hilo mbali na kuwa la uzinduzi, pia lilitoa fursa ya washiriki kuona fursa za uwekezaji mzuri na wa uhakika uliofanywa na makampuni hayo.

"Washiriki watapata fursa ya kujionea wenyewe uwekezaji unaohusu nyumba zenye chumba kimoja, viwili na hata vitatu, ambazo zinagharimu kati ya dola za Marekani 81,186, USD 147,427, na USD 191,838; zaidi ya hayo, wawekezaji hao watatoa punguzo la asilimia 8 ya bei ya kila nyumba kama ilivyoorodheshwa, ambapo punguzo hilo litahusu siku ya uzinduzi tu”, imesema taarifa ya pamoja iliyotolewa na uongozi ma makampuni hayo mawili.

Akiongea katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Coral property Holdings Li Jun, amesema, “Uwekezaji huu umelenga kuunga mkono juhudi za Serikali zinazolenga kuhakikisha kunakuwa na nyumba nzuri za makazi na zenye bei nafuu; kupitia miradi ya maendeleo kama vile Sky Royal, pia tunalenga si kuwekeza kwenye nyumba tu, bali pia kuhakikisha wananchi wanakuwa na maisha endelevu, yenye ufanisi na ambayo yatachangia ustawi wa familia kwa ajili ya Watanzania.”

Amesema kampuni yake pia imejikita katika kuhifadhi na kulinda mazingira nakwamba mpango huo ni endelevu. Aidha amesema mradi huo wa Sky Royal unahusu mpango kabambe wa kiteknolojia unaolenga uwekezji wa nyumba bora unaohakikisha mazingira rafiki na kwamba mradi huo umeidhinishwa kituo cha uwekezaji nchini TIC.

Naye, Mkurugenzi wa Kanda wa kampuni ya RE/MAX Pwani, James Prevost, amesema, “Ushirikiano wetu na kampuni ya Coral Property Holdings hususan katika mradi huu wa Sky Royal, umetuwezesha kuwapatia wananchi Jijini Dar es Salaam maisha bora kupitia nyumba nzuri za makazi na zenye unafuu; punguzo la bei siku hii ya uzinduzi pia ni wito kwa wateja kunufaika na uwekezji wa huu mzuri”.

Amesema mradi wa Sky Royal haulengi uwekezaji wa nyumba za makazi tu, bali pia ni kielelezo cha uwekezaji wa nyumba nzuri na za uhakika ambao unalenga kutoa makazi mazuri na endelevu kwa wananchi na kwa bei nafuu.

"Eneo la kimkakati la maendeleo na huduma kamili kwa jamii, inalenga kutengeneza mazingira bora kwa wataalamu wa aina malimbali wakiwemo vijana, kwa wanafamilia na wamiliki wa biashara aina mablimbali," amesema.

Kampuni ya RE/MAX Coastal inasifika kwa utaalamu wake katika maswala ya mauzo na masoko ya majengo, ikiwa na dhamira ya kuwapatia wateja kilicho bora na chenye thamani kulingana na soko lililoko nchini Tanzania.

Kampuni ya Coral Property Holdings imekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza uwekezaji wa uhakika wa majengo aina mbalimbali ikiwemo nyumba bora za makazi huku ikizingatia ubunifu wa hali ya juu na endelevu sambamba na ubora wa hali ya juu katika kuhakikisha kunakuweko na suluhisho la uhakika katika sekta ya makazi nchini Tanzania.

Ushirikiano kati ya RE/MAX Coastal na Coral Property Holdings kwenye uzinduzi wa mradi wa Sky Royal ni juhudi za kihistoria zinazolenga kuimarisha mandhari ya jiji la Dar es Salaam.

Kwa kuanisha malengo yao sambamba na ile ajenda ya Taifa inayolenga kuhakikisha uwepp wa makazi bora, kampuni zote mbili zimedhamiria kuimarisha sekta ya ujenzi hususani ujenzi wa majengo aina mbalimbali kwa lengo la kustawisha maisha ya Watanzania wote kwa ujumla.

Top News